Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 1:29-51

Yohana 1:29-51 NENO

Siku iliyofuata, Yahya alimwona Isa akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.” Kisha Yahya akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho Mtakatifu wa Mungu akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho Mtakatifu wa Mungu akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho wa Mungu.’ Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.” Siku iliyofuata, Yahya alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. Alipomwona Isa akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!” Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yahya akisema haya, wakamfuata Isa. Isa akageuka, akawaona wakimfuata, akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Mwalimu, unaishi wapi?” Isa akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!” Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yahya alisema na kumfuata Isa. Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masihi” (yaani Al-Masihi). Naye akamleta kwa Isa. Isa akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro). Siku iliyofuata Isa aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa raia wa Bethsaida, mji walikotoka Andrea na Petro. Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Torati, na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani Isa Al-Nasiri, mwana wa Yusufu.” Nathanaeli akauliza, “Nasiri! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nasiri?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.” Isa alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake, akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.” Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?” Isa akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.” Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!” Isa akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu kuliko hilo.” Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”