Yohana 1:1-9
Yohana 1:1-9 NENO
Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye. Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda. Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yahya. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.