Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 7

7
Dini za uongo ni batili
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu: 2“Simama kwenye lango la nyumba ya Mwenyezi Mungu, na huko upige mbiu ya ujumbe huu:
“ ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wote wa Yuda mliokuja kupitia malango haya ili kumwabudu Mwenyezi Mungu. 3Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Tengenezeni njia zenu na matendo yenu, nami nitawaacha mkae mahali hapa. 4Msitumainie maneno ya udanganyifu na kusema, “Hili ni Hekalu la Mwenyezi Mungu, Hekalu la Mwenyezi Mungu, Hekalu la Mwenyezi Mungu!” 5Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake, 6kama hamdhulumu mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama hamtafuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, 7ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele. 8Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.
9“ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, 10kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza? 11Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Mwenyezi Mungu.
12“ ‘Nendeni sasa mahali pangu palipokuwa huko Shilo, ambapo nilipafanya pa kwanza kuwa makao ya Jina langu, nanyi mwone lile nililopafanyia kwa ajili ya uovu wa watu wangu Israeli. 13Mlipokuwa mnafanya haya yote, asema Mwenyezi Mungu, nilisema nanyi tena na tena, lakini hamkusikiliza; niliwaita, lakini hamkujibu. 14Kwa hiyo, nililolifanyia Shilo, nitalifanya sasa kwa nyumba hii iitwayo kwa Jina langu, Hekalu mnalolitumainia, mahali nilipowapa ninyi na baba zenu. 15Nitawafukuza mbele yangu, kama nilivyowafanyia ndugu zenu, watu wa Efraimu.’
16“Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, wala usinililie, na usifanye maombi kwa ajili yao; usinisihi, kwa sababu sitakusikiliza. 17Je, huyaoni hayo wanayoyatenda katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu? 18Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto, na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha. 19Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asema Mwenyezi Mungu. Je, hawajiumizi wenyewe na kujiaibisha?
20“ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana Mungu Mwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu vitamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.
21“ ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe! 22Kwa kuwa nilipowaleta baba zenu kutoka Misri na kusema nao, sikuwapa amri kuhusu sadaka za kuteketezwa na dhabihu tu, 23lakini niliwapa amri hii nikisema: Nitiini mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Nendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa. 24Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Walirudi nyuma badala ya kusonga mbele. 25Tangu wakati ule baba zenu walipotoka Misri hadi sasa, siku baada ya siku, tena na tena nimewatumia watumishi wangu manabii. 26Lakini hawakunisikiliza wala hawakujali. Walikuwa na shingo ngumu na kufanya maovu kuliko baba zao.’
27“Utakapowaambia haya yote, hawatakusikiliza; utakapowaita, hawatajibu. 28Kwa hiyo waambie, ‘Hili ni taifa ambalo halimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wao, wala kukubali maonyo. Kweli imekufa, imetoweka midomoni mwao. 29Nyoeni nywele zenu na kuzitupa, ombolezeni katika miinuko iliyo kame, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekikataa na kukiacha kizazi hiki kilichomkasirisha.
Bonde la machinjo
30“ ‘Watu wa Yuda wamefanya maovu machoni pangu, asema Mwenyezi Mungu. Wameziweka sanamu zao za machukizo ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu, na wameitia unajisi. 31Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia sanamu pa Tofethi kwenye Bonde la Ben-Hinomu ili kuwateketeza watoto wao wa kiume na wa kike kwenye moto, kitu ambacho sikuamuru, wala hakikuingia akilini mwangu. 32Kwa hiyo mjihadhari, siku zinakuja, asema Mwenyezi Mungu, wakati watu watakapokuwa hawapaiti Tofethi au Bonde la Ben-Hinomu, lakini watapaita Bonde la Machinjo, kwa sababu watawazika wafu huko Tofethi hadi pasiwe tena nafasi. 33Ndipo mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwa na yeyote wa kuwafukuza. 34Nitazikomesha sauti za shangwe na furaha, na sauti za bwana arusi na bibi arusi katikati ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia