Yeremia 51
51
1Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi
dhidi ya Babeli na wenyeji wa Leb-Kamai#51:1 yaani Ukaldayo, Babeli kwa fumbo.
2Nitawatuma wageni Babeli
kumpepeta na kuiharibu nchi yake;
watampinga kila upande
katika siku ya maafa yake.
3Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake,
wala usimwache avae silaha zake.
Usiwaonee huruma vijana wake;
angamiza jeshi lake kabisa.
4Wataanguka barabarani waliouawa katika nchi ya Wakaldayo,
wakiwa na majeraha ya kutisha.
5Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa
na Mungu wao, Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
ingawa nchi yao imejaa uovu
mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
6“Kimbieni kutoka Babeli!
Okoeni maisha yenu!
Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake.
Ni wakati wa kisasi cha Mwenyezi Mungu,
atamlipa kile anachostahili.
7Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Mwenyezi Mungu;
aliufanya ulimwengu wote ulewe.
Mataifa walikunywa mvinyo wake;
kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.
8Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika.
Mwombolezeni!
Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake,
labda anaweza kupona.
9“ ‘Tungemponya Babeli,
lakini hawezi kuponyeka;
tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe,
kwa kuwa hukumu yake inafika angani,
inapanda juu hadi mawinguni.’
10“ ‘Mwenyezi Mungu amethibitisha haki yetu;
njooni, tutangaze katika Sayuni
kitu ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, amefanya.’
11“Noeni mishale,
chukueni ngao!
Mwenyezi Mungu amewaamsha wafalme wa Wamedi,
kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli.
Mwenyezi Mungu atalipiza kisasi,
kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
12Inueni bendera dhidi ya kuta za Babeli!
Imarisheni ulinzi,
wekeni walinzi,
andaeni waviziaji!
Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake,
amri yake juu ya watu wa Babeli.
13Wewe uishiye kando ya maji mengi
na uliye na wingi wa hazina,
mwisho wako umekuja,
wakati wako wa kukatiliwa mbali.
14Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:
‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige,
nao watashangilia kwa ushindi juu yako.’
15“Aliiumba dunia kwa uweza wake;
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
16Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
17“Kila mtu ni mjinga na hana maarifa;
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.
Vinyago vyake ni vya udanganyifu;
havina pumzi.
18Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha;
wakati wa hukumu yao, wataangamia.
19Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,
pamoja na kabila la urithi wake:
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
20“Wewe ndiwe rungu langu la vita,
silaha yangu ya vita:
kwa wewe navunjavunja mataifa,
kwa wewe naangamiza falme,
21kwa wewe navunjavunja
farasi na mpanda farasi,
kwa wewe navunjavunja
gari la vita na mwendeshaji wake,
22kwa wewe napondaponda
mwanaume na mwanamke,
kwa wewe napondaponda
mzee na kijana,
kwa wewe napondaponda
kijana wa kiume na mwanamwali,
23kwa wewe nampondaponda
mchungaji na kundi,
kwa wewe nampondaponda
mkulima na maksai,
kwa wewe nawapondaponda
watawala na maafisa.
24“Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote wanaoishi Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asema Mwenyezi Mungu.
25“Mimi niko kinyume nawe, ee mlima unaoharibu,
wewe uangamizaye dunia yote,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako,
nikuvingirishe kutoka kilele cha mwamba,
na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.
26Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako
kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni,
wala jiwe lolote kwa ajili ya msingi,
kwa maana utakuwa ukiwa milele,”
asema Mwenyezi Mungu.
27“Inueni bendera katika nchi!
Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa!
Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,
iteni falme hizi dhidi yake:
Ararati, Mini na Ashkenazi.
Wekeni jemadari dhidi yake,
pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.
28Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,
wafalme wa Wamedi,
watawala wao na maafisa wao wote,
pamoja na nchi zote wanazotawala.
29Nchi inatetemeka na kugaagaa,
kwa kuwa makusudi ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Babeli yanasimama:
yaani kuangamiza nchi ya Babeli
ili pasiwepo atakayeishi humo.
30Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana,
wamebaki katika ngome zao.
Nguvu zao zimekwisha,
wamekuwa kama wanawake.
Makazi yake yameteketezwa kwa moto,
makomeo ya malango yake yamevunjika.
31Tarishi mmoja humfuata mwingine,
na mjumbe humfuata mjumbe,
kumtangazia mfalme wa Babeli
kwamba mji wake wote umetekwa,
32Vivuko vya mito vimekamatwa,
mabwawa yenye mafunjo yametiwa moto,
nao askari wameingiwa na hofu kuu.”
33Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo:
“Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria
wakati inapokanyagwa;
wakati wa kumvuna utakuja upesi.”
34“Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula,
ametufanya tuchangayikiwe,
ametufanya tuwe gudulia tupu.
Ametumeza kama mnyama wa baharini,
na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri,
kisha akatutapika.
35Jeuri iliyotendewa miili yetu#51:35 au Jeuri tuliyotendewa sisi na watoto wetu na iwe juu ya Babeli,”
ndivyo wasemavyo wakaaji wa Sayuni.
“Damu yetu na iwe juu ya wakaaji wa Babeli,”
asema Yerusalemu.
36Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Tazama, nitakutetea
na kukulipizia kisasi;
nitaikausha bahari yake
na kuzikausha chemchemi zake.
37Babeli utakuwa lundo la magofu
na makao ya mbweha,
kitu cha kutisha na kudharauliwa,
mahali asipoishi mtu.
38Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo,
wanakoroma kama wana simba.
39Lakini wakiwa wameamshwa,
nitawaandalia karamu
na kuwafanya walewe,
ili washangilie kwa kicheko,
kisha walale milele na wasiamke,”
asema Mwenyezi Mungu.
40“Nitawateremsha kama wana-kondoo
wanaoenda machinjoni,
kama kondoo dume na mbuzi.
41“Tazama jinsi Sheshaki#51:41 Sheshaki ni Babeli kwa fumbo. atakavyokamatwa,
majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa.
Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani
kati ya mataifa!
42Bahari itainuka juu ya Babeli;
mawimbi yake yanayonguruma yatamfunika.
43Miji yake itakuwa ukiwa,
kame na jangwa,
nchi isiyokuwa na mtu anayeishi ndani yake,
ambayo hakuna mwanadamu atakayepita humo.
44Nitamwadhibu Beli katika Babeli,
na kumfanya atapike kitu alichokimeza.
Mataifa hayatamiminika tena kwake.
Nao ukuta wa Babeli utaanguka.
45“Tokeni ndani yake, enyi watu wangu!
Okoeni maisha yenu!
Ikimbieni hasira kali ya Mwenyezi Mungu.
46Msikate tamaa wala msiogope tetesi
zitakaposikika katika nchi;
tetesi moja inasikika mwaka huu,
nyingine mwaka unaofuata;
tetesi juu ya jeuri katika nchi,
na ya mtawala dhidi ya mtawala.
47Kwa kuwa hakika wakati utawadia
nitakapoziadhibu sanamu za Babeli;
nchi yake yote itatiwa aibu,
na watu wake wote waliouawa
wataangukia ndani yake.
48Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo
vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli,
kwa kuwa kutoka kaskazini
waangamizi watamshambulia,”
asema Mwenyezi Mungu.
49“Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli,
kama vile waliouawa duniani kote
walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.
50Wewe uliyepona upanga,
ondoka wala usikawie!
Mkumbuke Mwenyezi Mungu ukiwa katika nchi ya mbali,
na utafakari juu ya Yerusalemu.”
51“Tumetahayari, kwa sababu tumetukanwa
na aibu imefunika nyuso zetu,
kwa sababu wageni wameingia
mahali patakatifu pa nyumba ya Mwenyezi Mungu.”
52“Lakini siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu,
“nitakapoziadhibu sanamu zake,
na katika nchi yake yote
waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.
53Hata kama Babeli ikifika angani
na kuziimarisha ngome zake ndefu,
nitatuma waangamizi dhidi yake,”
asema Mwenyezi Mungu.
54“Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli,
sauti ya uharibifu mkuu
kutoka nchi ya Wakaldayo.
55Mwenyezi Mungu ataiangamiza Babeli,
atanyamazisha makelele ya kishindo chake.
Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu,
ngurumo ya sauti zao itavuma.
56Mwangamizi atakuja dhidi ya Babeli;
mashujaa wake watakamatwa,
nazo pinde zao zitavunjwa.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kisasi,
yeye atalipiza kikamilifu.
57Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe,
watawala wao, maafisa, pamoja na mashujaa wao;
watalala milele na hawataamka,”
asema Mfalme, ambaye jina lake ni Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni.
58Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa,
na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto;
mataifa yanajichosha bure,
taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”
59Huu ndio ujumbe ambao nabii Yeremia alimpa msimamizi wa nyumba ya mfalme, Seraya mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake. 60Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli. 61Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa. 62Kisha sema, ‘Ee Mwenyezi Mungu, umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’ 63Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati. 64Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ”
Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 51: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.