Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 34:8-22

Yeremia 34:8-22 NEN

Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa. Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa. Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru. Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema, ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali. Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu. Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena. “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo BWANA: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema BWANA: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia. Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama. Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama, nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu. Nitatoa amri, asema BWANA, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”