Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 29

29
Barua kwa watu wa uhamisho
1Haya ndio maneno ya barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa waliopelekwa uhamishoni, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu. 2(Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia#29:2 au Konia; pia anaitwa Yehoyakini na mama malkia, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.) 3Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:
4Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: 5“Jengeni nyumba na mwishi humo, pandeni bustani na mle mazao yake. 6Oeni wake na mzae watoto wa kiume na wa kike; watafutieni wake watoto wenu wa kiume, na waozeni binti zenu ili nao wazae watoto wa kiume na wa kike; mkaongezeke huko, wala msipungue idadi. 7Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
8Naam, hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na waaguzi walio miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. 9Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Mwenyezi Mungu.
10Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Mwenyezi Mungu, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wote. 14Nitaonekana kwenu,” asema Mwenyezi Mungu, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali nilipokuwa nimewatoa walipopelekwa uhamishoni,” asema Mwenyezi Mungu.
15Mnaweza mkasema, “Mwenyezi Mungu ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,” 16lakini hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu mfalme aketiye katika kiti cha utawala cha Daudi, na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, ndugu zenu ambao hawakuenda pamoja nanyi uhamishoni. 17Naam, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu zilizooza, zisizofaa kuliwa. 18Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni, nami nitawafanya kuwa chukizo kwa falme zote za dunia, kitu cha laana na cha kutisha, kisichofaa na cha kuzomewa miongoni mwa mataifa nitakakowafukuzia. 19Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema Mwenyezi Mungu, “maneno niliyoyatuma kwao mara kwa mara kupitia kwa watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema Mwenyezi Mungu.
20Kwa hiyo, sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi nyote mlio uhamishoni, niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu. 21Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya, na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa. 22Kwa ajili yao, watu wote wa Yuda walio uhamishoni Babeli watatumia laana hii: ‘Mwenyezi Mungu na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma moto.’ 23Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya. Nami nayajua haya, na ni shahidi wa jambo hilo,” asema Mwenyezi Mungu.
Ujumbe kwa Shemaya
24Mwambie Shemaya Mnehelami, 25“Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania, 26‘Mwenyezi Mungu amekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada ili uwe msimamizi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu. Unapaswa kumfunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu yeyote anayejifanya nabii. 27Kwa nini basi hukumkemea Yeremia Mwanathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu? 28Ametutumia ujumbe huu huku Babeli: Mtakuwa huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae; pandeni mashamba na mle mazao yake.’ ”
29Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua. 30Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 31“Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni kusema: ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo, 32hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Hakika nitamwadhibu Shemaya Mnehelami pamoja na uzao wake. Hapatakuwa na yeyote atakayebaki miongoni mwa watu hawa, wala hataona mema nitakayowatendea watu wangu, asema Mwenyezi Mungu, kwa sababu ametangaza uasi dhidi yangu.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 29: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia