Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 22:1-9

Yeremia 22:1-9 NEN

Hili ndilo asemalo BWANA: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko: ‘Sikia neno la BWANA, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha enzi cha Daudi: wewe, maafisa wako na watu wako mnaopitia malango haya. Hili ndilo BWANA asemalo: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. Kwa kuwa ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, ndipo wafalme watakaokalia kiti cha enzi cha Daudi watakapoingia kupitia malango ya jumba hili la kifalme, wakiwa wamepanda magari na farasi, huku wakifuatana na maafisa wao na watu wao. Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema BWANA, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ” Kwa kuwa hili ndilo BWANA asemalo kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda: “Ingawa uko kama Gileadi kwangu, kama kilele cha Lebanoni, hakika nitakufanya uwe kama jangwa, kama miji ambayo haijakaliwa na watu. Nitawatuma waharabu dhidi yako, kila mtu akiwa na silaha zake, nao watazikata boriti zako nzuri za mierezi na kuzitupa motoni. “Watu kutoka mataifa mengi watapitia karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini BWANA amefanya jambo la namna hii juu ya mji huu mkubwa?’ Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la BWANA, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ”