Yeremia 17
17
Dhambi ya Yuda na adhabu yake
1“Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma,
imeandikwa kwa ncha ya almasi,
kwenye vibao vya mioyo yao
na kwenye pembe za madhabahu zao.
2Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao
na nguzo za Ashera
kandokando ya miti iliyotanda
na juu ya vilima virefu.
3Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri
na hazina zako zote nitavitoa viwe nyara,
pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia
kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.
4Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza
urithi niliokupa.
Nitakufanya mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa umeiwasha hasira yangu,
nayo itawaka milele.”
5Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,
amtegemeaye mwenye mwili
kwa ajili ya nguvu zake,
ambaye moyo wake
umemwacha Mwenyezi Mungu.
6Atakuwa kama kichaka cha jangwani;
hataona mafanikio yatakapokuja.
Ataishi katika sehemu zisizo na maji,
katika nchi ya chumvi ambapo
hakuna yeyote aishiye humo.
7“Lakini amebarikiwa mtu anayemtumaini Mwenyezi Mungu,
ambaye matumaini yake ni katika Mwenyezi Mungu.
8Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji
uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.
Hauogopi wakati wa joto ujapo;
majani yake ni mabichi daima.
Hauna hofu katika mwaka wa ukame
na hautaacha kuzaa matunda.”
9Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,
ni mwovu kupita kiasi.
Ni nani awezaye kuujua?
10“Mimi Mwenyezi Mungu ninauchunguza moyo
na kuzijaribu nia,
ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,
kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”
11Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga,
ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki.
Maisha yake yatakapofika katikati, siku zitamwacha,
na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
12Kiti cha enzi kilichotukuzwa, kilichoinuliwa tangu mwanzo,
ndiyo sehemu yetu ya mahali patakatifu.
13Ee Mwenyezi Mungu, uliye tumaini la Israeli,
wote wakuachao wataaibika.
Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini
kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu,
chemchemi ya maji yaliyo hai.
14Uniponye, Ee Mwenyezi Mungu, nami nitaponyeka;
uniokoe nami nitaokoka,
kwa maana wewe ndiwe ninayekusifu.
15Wao huendelea kuniambia,
“Liko wapi neno la Mwenyezi Mungu?
Sasa na litimie!”
16Sijakukimbia na kuacha kuwa mchungaji wako;
unajua sijaitamani siku ya kukata tamaa.
Kile kipitacho mdomoni mwangu
ki wazi mbele yako.
17Usiwe kwangu kitu cha kunitia hofu kuu;
wewe ndiwe kimbilio langu katika siku ya maafa.
18Watesi wangu na waaibishwe,
lakini nilinde mimi nisiaibike;
wao na watiwe hofu kuu,
lakini unilinde mimi na hofu kuu.
Waletee siku ya maafa;
waangamize kwa maangamizi maradufu.
Kuiadhimisha Sabato
19Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nenda ukasimame kwenye lango la watu, mahali ambako wafalme wa Yuda huingilia na kutokea; simama pia kwenye malango mengine yote ya Yerusalemu. 20Waambie, ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wote wa Yuda, na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya. 21Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu. 22Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yoyote siku ya Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu. 23Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao, na hawakutaka kusikia wala kukubali adhabu. 24Lakini mkiwa waangalifu kunitii, asema Mwenyezi Mungu, nanyi msipoleta mzigo wowote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo, 25ndipo wafalme wanaokaa kwenye kiti cha utawala cha Daudi wataingia kupitia malango ya mji huu, pamoja na maafisa wao. Wafalme na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari ya vita na farasi, wakiandamana na watu wote wa Yuda na wakaaji wa Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima. 26Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na Shefela#17:26 au upande wa magharibi chini ya vilima, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu. 27Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wowote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.