Waamuzi 8
8
Ushindi Wa Gideoni Na Kulipiza Kisasi
1 Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona mmetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakawalaumu kwa ukali sana.
2 Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri? 3 Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.
4 Gideoni akiwa pamoja na wale watu 300 waliofuatana naye, wakiwa wamechoka na wenye njaa lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka. 5 Akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”
6 Lakini maafisa wa Sukothi wakasema, “Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?”
7Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, Bwana atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”
8 Kutoka hapo alikwea mpaka Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao watu wa Penieli wakamjibu kama watu wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu. 9Hivyo akawaambia watu wa Penieli, “Nitakaporudi baada ya kushinda, nitaubomoa mnara huu.”
10 Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori wakiwa na jeshi lenye watu wapatao 15,000 wale wote waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao 120,000 wenye panga walikuwa wameuawa. 11 Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wasafiri mashariki ya Noba na Yogbeha na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote. 12Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote.
13 Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kwa kupitia Mwinuko wa Heresi. 14 Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya maafisa sabini wa Sukothi, ambao ni viongozi wa mji. 15Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia watu wa Sukothi, “Tazama, hapa wapo Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?’ ” 16 Akawachukua hao viongozi wa mji na kuwafundisha watu wa Sukothi somo kwa kuwaadhibu kwa miiba na michongoma ya nyikani. 17Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua watu wa mji.
18 Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni watu wa aina gani mliowaua huko Tabori?”
Wakajibu, “Ni watu kama wewe, kila mmoja wao akiwa na nafasi ya uana wa mfalme.”
19 Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama aishivyo Bwana, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.” 20Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.
21 Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mtu, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo Gideoni akatoka mbele na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia zao.
Kisibau Cha Gideoni
22Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, wanao na wana wa wana wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”
23 Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitatawala juu yenu, wala wanangu hawatatawala juu yenu. Bwana ndiye atakayetawala juu yenu ninyi.” 24 Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka kwenye fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
25Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka kwenye fungu lake la nyara. 26Uzito wa pete za dhahabu alizoomba zilifikia shekeli 1,700,#8:26 Shekeli 1,700 ni sawa na kilo 19.5. bila kuhesabu mapambo mengine, pete za masikio na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia zao. 27 Gideoni akatengeneza kisibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani, Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
28 Hivyo Midiani ikashindwa mbele ya Israeli nayo haikuinua kichwa chake tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.
Kifo Cha Gideoni
29 Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake. 30 Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi. 31 Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, ambaye alimwita Abimeleki. 32 Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, na akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.
33 Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na 34 wala hawakumkumbuka Bwana Mungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande. 35 Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanya kwa ajili yao.
Iliyochaguliwa sasa
Waamuzi 8: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.