Yakobo 4
4
Jinyenyekezeni kwa Mwenyezi Mungu
1Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.
4Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5Au mwadhani kwamba Maandiko yasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Maandiko yasema:
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”#4:6 Mithali 3:34
7Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9Huzunikeni, na mwomboleze, na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10Jinyenyekezeni mbele za Mwenyezi Mungu, naye atawainua.
Onyo kuhusu kuwahukumu wengine
11Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu, anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria, bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria. 12Yuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu; ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?
Kujivuna kwa ajili ya kesho
13Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutaenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Mwenyezi Mungu akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16Ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kote kwa namna hii ni uovu. 17Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
Iliyochaguliwa sasa
Yakobo 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.