Yakobo 4:1-12
Yakobo 4:1-12 NEN
Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu. Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua. Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria. Yuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu, ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?