Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yakobo 1

1
Salamu
1Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Isa Al-Masihi.
Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni.
Salamu.
Imani na hekima
2Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4Acheni saburi ikamilishe kazi yake, ili mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. 5Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima, basi amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, linalopeperushwa na upepo na kutupwa huku na huko. 7Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana Isa. 8Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.
Umaskini na utajiri
9Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. 10Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. 11Kwa maana jua kali huchomoza na kuyakausha majani ya mmea, nalo ua lake linaanguka, na uzuri wake unaharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.
Kujaribiwa
12Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji lile la uzima Mungu alilowaahidia wale wanaompenda.
13Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa huzaa mauti.
16Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. 17Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. 18Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.
Kusikia na kutenda
19Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. 20Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.
22Basi kuweni watendaji wa Neno, wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na husahau upesi jinsi alivyo. 25Lakini yeye anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau, bali akatenda alichosikia, basi atabarikiwa katika kile anachofanya.
26Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake haifai kitu. 27Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu, Baba#1:27 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, ndiyo hii: ni kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

Iliyochaguliwa sasa

Yakobo 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia