Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 8:1-10

Isaya 8:1-10 NENO

Mwenyezi Mungu akaniambia, “Chukua kitabu kikubwa, uandike kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi. Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.” Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi. Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.” Mwenyezi Mungu akasema nami tena: “Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yanayotiririka taratibu wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia; kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao mafuriko makubwa ya Mto: yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote. Yatafurika juu ya mifereji yake yote, yatamwagikia juu ya kingo zake zote, na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake, yakipita katikati na yakifika hadi shingoni. Mabawa yake yaliyokunjuliwa yatafunika upana wa nchi yako, Ee Imanueli!” Inueni ukelele wa vita, enyi mataifa, na mkavunjwevunjwe! Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali. Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa; fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa, kwa maana Mungu yu pamoja nasi.