Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 7:1-17

Isaya 7:1-17 NEN

Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda. Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo. Ndipo BWANA akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi. Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia. Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema, “Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.” Lakini BWANA Mwenyezi asema hivi: “ ‘Jambo hili halitatendeka, halitatokea, kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake. Katika muda wa miaka sitini na mitano, Efraimu atakuwa ameharibiwa kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa. Kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia peke yake. Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu, hamtaimarika kamwe.’ ” BWANA akasema na Ahazi tena, “Mwombe BWANA Mungu wako ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.” Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu BWANA.” Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli. Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema. Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa. BWANA ataleta juu yako, juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: yeye atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”