Isaya 60:1-6
Isaya 60:1-6 NEN
“Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa BWANA umezuka juu yako. Tazama, giza litaifunika dunia na giza kuu litayafunika mataifa, lakini BWANA atazuka juu yako na utukufu wake utaonekana juu yako. Mataifa watakuja kwenye nuru yako na wafalme kwa mwanga wa mapambazuko yako. “Inua macho yako na utazame pande zote: Wote wanakusanyika na kukujia, wana wako wanakuja toka mbali, nao binti zako wanabebwa mikononi. Ndipo utatazama na kutiwa nuru, moyo wako utasisimka na kujaa furaha, mali zilizo baharini zitaletwa kwako, utajiri wa mataifa utakujilia. Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako, ngamia vijana wa Midiani na Efa. Nao wote watokao Sheba watakuja, wakichukua dhahabu na uvumba na kutangaza sifa za BWANA.