Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 5

5
Wimbo wa shamba la mizabibu
1Nitaimba wimbo kwa mpenzi wangu,
wimbo kuhusu shamba lake la mizabibu:
Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu
kwenye kilima chenye rutuba.
2Alililima na kuondoa mawe
na akaliotesha mizabibu bora sana.
Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake,
na kutengeneza shinikizo la kukamulia zabibu pia.
Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri,
lakini lilizaa matunda mabaya tu.
3“Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,
hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.
4Ni nini zaidi ambacho kingefanyika katika shamba langu la mizabibu
kuliko yale niliyofanya?
Nilipotazamia kupata zabibu nzuri,
kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?
5Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea
shamba langu la mizabibu:
Nitaondoa uzio wake,
nalo litaharibiwa,
nitabomoa ukuta wake,
nalo litakanyagwa.
6Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,
halitakatiwa matawi wala kulimwa,
nayo michongoma na miiba itamea huko,
nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”
7Shamba la mzabibu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
ni nyumba ya Israeli,
na watu wa Yuda
ni bustani yake ya kumpendeza.
Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu;
alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.
Ole na hukumu
8Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba
na kuunganisha mashamba baada ya mashamba
hadi hakuna nafasi iliyobaki,
nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
9Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amesema nikisikia:
“Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa,
nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
10Shamba la mizabibu la eka kumi
litatoa bathi moja#5:10 Bathi moja ni sawa na lita 22. ya divai,
na homeri moja#5:10 Homeri moja ni sawa na lita 220. ya mbegu zilizopandwa
itatoa efa moja#5:10 Efa moja ni sawa na lita 22. tu ya nafaka.”
11Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema
wakikimbilia kunywa vileo,
wale wakawiao sana hadi usiku,
hata wamewaka kwa mvinyo.
12Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,
matari, filimbi na mvinyo,
lakini hawayajali matendo ya Mwenyezi Mungu,
wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
13Kwa hiyo watu wangu wataenda uhamishoni
kwa sababu ya kukosa maarifa;
watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa,
nao watu wengi watakauka kwa kiu.
14Kwa hiyo Kaburi#5:14 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol. limeongeza hamu yake
na kupanua mdomo wake bila kikomo,
ndani yake watashuka wakuu wao na wingi wa watu,
pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.
15Hivyo mwanadamu atashushwa,
na binadamu kunyenyekezwa,
macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
16Lakini Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atatukuzwa
kwa ajili ya haki yake,
naye Mungu Mtakatifu atajionesha mwenyewe
kuwa mtakatifu kwa haki yake.
17Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe,
wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri.
18Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu
na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,
19kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka,
aharakishe kazi yake ili tupate kuiona.
Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike,
tena udhihirike ili tupate kuujua.”
20Ole wao wanaoita ubaya ni wema,
na wema ni ubaya,
wawekao giza badala ya nuru,
na nuru badala ya giza,
wawekao uchungu badala ya utamu,
na utamu badala ya uchungu.
21Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe,
na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.
22Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo,
nao walio hodari katika kuchanganya vileo,
23wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,
lakini huwanyima haki wasio na hatia.
24Kwa hiyo, kama ndimi za moto zinavyoteketeza nyasi,
na kama vile majani makavu yanavyozama katika miali ya moto,
ndivyo mizizi yao itakavyooza,
na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi;
kwa kuwa wameikataa Torati ya Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni
na kulisukumia mbali neno la
Aliye Mtakatifu wa Israeli.
25Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu
inawaka dhidi ya watu wake,
mkono wake umeinuliwa na anawapiga.
Milima inatetemeka,
maiti ni kama takataka kwenye barabara.
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
26Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali,
anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia.
Tazama wamekuja,
kwa kasi na kwa haraka!
27Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa,
hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala,
hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni,
hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.
28Mishale yao ni mikali,
pinde zao zote zimevutwa,
kwato za farasi wao ziko kama gumegume,
magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.
29Ngurumo yao ni kama ile ya simba,
wananguruma kama wana simba,
wanakoroma wanapokamata mawindo yao,
na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa.
30Katika siku ile watanguruma juu yake
kama ngurumo za bahari.
Kama mtu akiitazama nchi,
ataona giza na dhiki;
hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia