Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 46

46
Miungu ya Babeli
1Beli anasujudu, Nebo anainama;
sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo.
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,
mzigo kwa waliochoka.
2Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,
wote wanaenda utumwani pamoja.
3“Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo,
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.
4Hata wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.
Nimewahuluku, nami nitawabeba,
nitawahudumia ninyi na kuwaokoa.
5“Mtanilinganisha na nani,
au mtanihesabu kuwa sawa na nani?
Ni nani mtakayenifananisha naye
ili tuweze kulinganishwa?
6Wengine humwaga dhahabu kutoka mifuko yao,
na kupima fedha kwenye mizani;
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,
kisha huisujudia na kuiabudu.
7Huiinua mabegani na kuichukua;
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.
Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.
Ingawa mtu huililia, haimjibu;
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.
8“Kumbukeni hili, litieni akilini,
liwekeni moyoni, enyi waasi.
9Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;
mimi ndimi Mungu,
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
10Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,
naam, tangu zamani za kale,
mambo ambayo hayajatendeka.
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;
kutoka nchi ya mbali,
mtu atakayetimiza kusudi langu.
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;
lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.
12Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,
ninyi mlio mbali na haki.
13Ninaleta haki yangu karibu,
haiko mbali;
wala wokovu wangu hautachelewa.
Nitawapa Sayuni wokovu,
Israeli utukufu wangu.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 46: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia