Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 43:14-28

Isaya 43:14-28 NEN

Hili ndilo BWANA asemalo, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa ajili yenu nitatumana Babeli na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi, katika meli walizozionea fahari. Mimi ndimi BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wako, Muumba wa Israeli, Mfalme wako.” Hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyefanya njia baharini, mahali pa kupita kwenye maji mengi, aliyeyakokota magari ya vita na farasi, jeshi pamoja na askari wa msaada, nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe, wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi: “Msiyakumbuke mambo yaliyopita, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitafanya jambo jipya! Sasa litachipuka, je, hamtalitambua? Nitafanya njia jangwani na vijito vya maji katika nchi kame. Wanyama wa mwituni wataniheshimu, mbweha na bundi, kwa sababu ninawapatia maji jangwani, na vijito katika nchi kame, ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua, watu wale niliowaumba kwa ajili yangu, ili wapate kutangaza sifa zangu. “Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo, hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli. Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukulemea kwa sadaka za nafaka wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba. Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato, wala hukunipa kwa ukarimu mafuta ya wanyama wa dhabihu zako. Lakini umenilemea kwa dhambi zako, na kunitaabisha kwa makosa yako. “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako, kwa ajili yangu mwenyewe, wala sizikumbuki dhambi zako tena. Tafakari mambo yaliyopita, njoo na tuhojiane, leta shauri lako uweze kupewa haki yako. Baba yako wa kwanza alitenda dhambi, wasemaji wako wameasi dhidi yangu. Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako, nami nitamtoa Yakobo aangamizwe, na Israeli adhihakiwe.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha