Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 36

36
Senakeribu atishia Yerusalemu
(2 Wafalme 18:13-27; 2 Nyakati 32:1-19)
1Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. 2Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wa jeshi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Jemadari wa jeshi akasimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. 3Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea.
4Jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia,
“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? 5Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? 6Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. 7Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu”: Je, si yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya”?
8“ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! 9Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? 10Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
11Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
12Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”
13Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 14Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa! 15Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Mwenyezi Mungu kwa kuwaambia, ‘Hakika Mwenyezi Mungu atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
16“Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, 17hadi nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu.
18“Msikubali Hezekia awapotoshe asemapo, ‘Mwenyezi Mungu atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 19Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? 20Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mwenyezi Mungu aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
21Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
22Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia vile jemadari wa jeshi alivyosema.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 36: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia