Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 28:14-22

Isaya 28:14-22 NEN

Kwa hiyo sikieni neno la BWANA, enyi watu wenye dharau mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu. Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti, tumefanya mapatano na kuzimu. Wakati pigo lifurikalo litakapopita, haliwezi kutugusa sisi, kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.” Kwa hiyo hivi ndivyo BWANA Mwenyezi asemavyo: “Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti. Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu. Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia na uadilifu kuwa timazi; mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo, nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha. Agano lenu na kifo litabatilishwa, patano lenu na kuzimu halitasimama. Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba, litawaangusha chini. Kila mara lijapo litawachukua, asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku, litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.” Kuuelewa ujumbe huu utaleta hofu tupu. Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake, nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno mtu hawezi kujifunikia. BWANA atainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu, ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni: ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu, ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni. Sasa acheni dharau zenu, la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi. Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, ameniambia habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote.