Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 26

26
Wimbo wa ushindi
1Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:
Tuna mji ulio na nguvu,
Mungu huufanya wokovu
kuwa kuta zake na maboma yake.
2Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,
taifa lidumishalo imani.
3Utamlinda katika amani kamilifu
yeye ambaye moyo wake ni thabiti
kwa sababu anakutumaini wewe.
4Mtumaini Mwenyezi Mungu milele,
kwa kuwa Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu,
ni Mwamba wa milele.
5Huwashusha wale wajikwezao,
huushusha chini mji wenye kiburi,
huushusha hadi ardhini
na kuutupa chini mavumbini.
6Miguu huukanyagia chini:
miguu ya hao waliodhulumiwa,
hatua za hao maskini.
7Mapito ya wenye haki ni nyoofu.
Ewe uliye Mwenye Haki,
waisawazisha njia ya mtu mnyofu.
8Naam, Mwenyezi Mungu, tukienenda katika sheria zako,
twakungojea wewe,
jina lako na sifa zako
ndizo shauku za mioyo yetu.
9Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,
wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.
Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,
watu wa ulimwengu hujifunza haki.
10Ingawa neema yaoneshwa kwa waovu,
hawajifunzi haki;
hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya
wala hawazingatii utukufu wa Mwenyezi Mungu.
11Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako umeinuliwa juu,
lakini hawauoni.
Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe,
moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.
12Mwenyezi Mungu, unaamuru amani kwa ajili yetu,
yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.
13Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala,
lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.
14Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai,
roho za waliokufa hazitarudi tena.
Uliwaadhibu na kuwaangamiza,
umefuta kumbukumbu lao lote.
15Umeliongeza hilo taifa, Ee Mwenyezi Mungu,
umeliongeza hilo taifa.
Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe,
umepanua mipaka yote ya nchi.
16Mwenyezi Mungu, walikujia katika taabu yao,
wewe ulipowarudi,
waliweza kuomba kwa kunong’ona tu.
17Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa
anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake,
ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Mwenyezi Mungu.
18Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu,
lakini tulizaa upepo.
Hatukuleta wokovu duniani,
hatujazaa watu katika ulimwengu huu.
19Lakini wafu wenu wataishi,
nayo miili yao itafufuka.
Ninyi mnaokaa katika mavumbi,
amkeni mkashangilie kwa furaha.
Umande wenu ni kama umande wa asubuhi,
dunia itawazaa wafu wake.
20Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu
na mfunge milango nyuma yenu,
jificheni kwa kitambo kidogo
hadi ghadhabu yake ipite.
21Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja kutoka makao yake
ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao.
Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake,
wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 26: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia