Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 22

22
Unabii kuhusu Yerusalemu
1Neno la unabii kuhusu Bonde la Maono:
Nini kinachokutaabisha sasa,
kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?
2Ewe mji uliojaa ghasia,
ewe mji wa makelele na sherehe!
Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,
wala hawakufa vitani.
3Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,
wamekamatwa bila kutumia upinde.
Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,
mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.
4Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,
niache nilie kwa uchungu.
Usijaribu kunifariji
juu ya maangamizi ya watu wangu.”
5Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayo siku
ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya
katika Bonde la Maono,
siku ya kuangusha kuta
na ya kupiga kelele hadi milimani.
6Elamu analichukua podo,
pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.
Kiri anaifungua ngao.
7Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,
nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji.
8Ulinzi wa Yuda umeondolewa.
Nawe ulitazama siku ile
silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni.
9Mkaona kuwa Mji wa Daudi
una matundu mengi katika ulinzi wake,
mkaweka akiba ya maji
kwenye Bwawa la Chini.
10Mlihesabu majengo katika Yerusalemu
nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.
11Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili
kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,
lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,
au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.
12Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
aliwaita siku ile
ili kulia na kuomboleza,
kung’oa nywele zenu na kuvaa magunia.
13Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,
kuchinja ng’ombe na kuchinja kondoo,
kula nyama na kunywa mvinyo!
Mnasema, “Tuleni na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa!”
14Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amelifunua hili nikiwa ninasikia: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema: “Hadi siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”
15Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo:
“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,
ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:
16Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa
kujikatia kaburi lako mwenyewe,
ukichonga kaburi lako mahali palipo juu,
na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?
17“Jihadhari, Mwenyezi Mungu yu karibu kukukamata thabiti,
na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.
18Atakuvingirisha uwe kama mpira
na kukutupa katika nchi kubwa.
Huko ndiko utakakofia,
na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,
na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako!
19Nitakuondoa kutoka kazi yako,
nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.
20“Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. 21Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. 22Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. 23Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. 24Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”
25Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioning’inia juu yake utaanguka chini.” Mwenyezi Mungu amesema.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia