Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 14

14
Yuda Kufanywa Upya
1 Bwana atamhurumia Yakobo,
atamchagua Israeli tena,
na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe.
Wageni wataungana nao
na kujiunga na nyumba ya Yakobo.
2 Mataifa watawachukua
na kuwaleta mahali pao wenyewe.
Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa
kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana.
Watawafanya watekaji wao kuwa mateka,
na kutawala juu ya wale waliowaonea.
3 Katika siku Bwana atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili, 4 utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli:
Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho!
Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!
5 Bwana amevunja fimbo ya mwovu,
fimbo ya utawala ya watawala,
6 ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa
kwa mapigo yasiyo na kikomo,
nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa
kwa jeuri pasipo huruma.
7 Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani,
wanabubujika kwa kuimba.
8 Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni
inashangilia mbele yako na kusema,
“Basi kwa sababu umeangushwa chini,
hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”
9 Kuzimu kote kumetaharuki
kukulaki unapokuja,
kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea,
wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu,
kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme:
wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.
10 Wote wataitikia,
watakuambia,
“Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo;
wewe umekuwa kama sisi.”
11 Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu,
pamoja na kelele ya vinubi vyako,
mafunza yametanda chini yako,
na minyoo imekufunika.
12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,
ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!
Umetupwa chini duniani,
wewe uliyepata kuangusha mataifa!
13 Ulisema moyoni mwako,
“Nitapanda juu hadi mbinguni,
nitakiinua kiti changu cha enzi
juu ya nyota za Mungu,
nitaketi nimetawazwa
juu ya mlima wa kusanyiko,
kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.
14 Nitapaa juu kupita mawingu,
nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”
15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,
hadi kwenye vina vya shimo.
16 Wale wanaokuona wanakukazia macho,
wanatafakari hatima yako:
“Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia
na kufanya falme zitetemeke,
17 yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa,
aliyeipindua miji yake,
na ambaye hakuwaachia mateka wake
waende nyumbani?”
18 Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima
kila mmoja katika kaburi lake.
19 Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako
kama tawi lililokataliwa,
umefunikwa na waliouawa
pamoja na wale waliochomwa kwa upanga,
wale washukao mpaka
kwenye mawe ya shimo.
Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,
20 Hutajumuika nao kwenye mazishi,
kwa kuwa umeharibu nchi yako
na kuwaua watu wako.
Mzao wa mwovu
hatatajwa tena kamwe.
21 Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe
kwa ajili ya dhambi za baba zao,
wasije wakainuka ili kuirithi nchi
na kuijaza dunia kwa miji yao.
22 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema,
“Nitainuka dhidi yao,
nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika,
watoto wake na wazao wake,”
asema Bwana.
23 “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi,
na kuwa nchi ya matope;
nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,”
asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Unabii Dhidi Ya Ashuru
24 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa,
“Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,
nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.
25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,
juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.
Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,
nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”
26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,
huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.
27 Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia,
ni nani awezaye kumzuia?
Mkono wake umenyooshwa,
ni nani awezaye kuurudisha?
Unabii Dhidi Ya Wafilisti
28Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:
29 Msifurahi, enyi Wafilisti wote,
kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika;
kutoka mzizi wa huyo nyoka
atachipuka nyoka mwenye sumu kali,
uzao wake utakuwa joka lirukalo,
lenye sumu kali.
30 Maskini kuliko maskini wote watapata malisho,
nao wahitaji watalala salama.
Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa,
nayo njaa itawaua walionusurika.
31 Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji!
Yeyukeni, enyi Wafilisti wote!
Wingu la moshi linakuja toka kaskazini,
wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.
32 Ni jibu gani litakalotolewa
kwa wajumbe wa taifa hilo?
Bwana ameifanya imara Sayuni,
nako ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 14: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia