Isaya 10:12-21
Isaya 10:12-21 NENO
Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao. Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ” Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia! Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa mashujaa wake wanene, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto. Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake. Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo. Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu. Katika siku ile, mabaki ya Israeli, walionusurika wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, lakini watamtegemea kwa kweli Mwenyezi Mungu Aliye Mtakatifu wa Israeli. Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.