Hosea 2:14-23
Hosea 2:14-23 NEN
“Kwa hiyo sasa nitamshawishi; nitamwongoza hadi jangwani na kuzungumza naye kwa upole. Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, nami nitalifanya Bonde la Akori mlango wa matumaini. Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama siku zile alizotoka Misri. “Katika siku ile,” asema BWANA, “utaniita mimi ‘Mume wangu’; hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’ Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka midomoni mwake, wala hataomba tena kwa majina yao. Katika siku ile nitafanya Agano kwa ajili yao na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani, na viumbe vile vitambaavyo ardhini. Upinde, upanga na vita, nitaondolea mbali katika nchi, ili kwamba wote waweze kukaa salama. Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma. Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali BWANA. “Katika siku ile nitajibu,” asema BWANA, “nitajibu kwa anga, nazo anga zitajibu kwa nchi; nayo nchi itajibu kwa nafaka, divai mpya na mafuta, navyo vitajibu kwa Yezreeli. Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitaonyesha pendo langu kwake yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu.’ Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu,’ ‘Ninyi ni watu wangu’; nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”