Waebrania 12:1-9
Waebrania 12:1-9 NEN
Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa. Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usikate tamaa akikukemea, kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.” Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?