Mwanzo 47:1-12
Mwanzo 47:1-12 NEN
Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wapo huko Gosheni.” Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao. Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.” Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.” Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako, nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu yeyote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.” Ndipo Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao, Farao akamuuliza, “Je una umri gani?” Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya kusafiri ya baba zangu.” Kisha Yakobo akambariki Farao, naye akaondoka mbele ya uso wake. Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza. Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.