Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45:1-15

Mwanzo 45:1-15 NENO

Basi Yusufu hakuweza kujizuia tena mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye. Akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwa mtu mwingine na Yusufu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari. Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yusufu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake. Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yusufu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa njaa imekuwa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwa na kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu. “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kama baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. Sasa rudini haraka kwa baba yangu, mkamwambie, ‘Hili ndilo mwanao Yusufu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa mtawala wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami: wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’ “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. Mwambieni baba yangu kuhusu heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.” Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo, ndugu zake wakazungumza naye.