Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 42:1-13

Mwanzo 42:1-13 NENO

Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka kule Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mkitazamana?” Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Teremkeni huko mkatununulie chakula, ili tuweze kuishi wala tusife.” Ndipo ndugu kumi wa Yusufu wakateremka huko Misri kununua nafaka. Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yusufu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara. Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale walioenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia. Wakati huo Yusufu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, na ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yusufu walifika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi. Mara Yusufu alipowaona ndugu zake, akawatambua. Lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.” Ingawa Yusufu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua. Ndipo Yusufu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.” Wakamjibu, “Sivyo, bwana. Watumishi wako wamekuja kununua chakula. Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.” Akawaambia, “La, hasha! Mmekuja kuangalia mahali nchi yetu haina ulinzi.” Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu, na mwingine alikufa.”