Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:28-45

Mwanzo 41:28-45 NENO

“Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri, lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi. “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni. “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe. Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.” Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. Hivyo Farao akawauliza, “Je, tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, aliye na Roho wa Mungu ndani yake?” Ndipo Farao akamwambia Yusufu, “Maadamu Mungu amekufunulia haya yote, hakuna yeyote mwenye akili na hekima kama wewe. Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.” Kwa hiyo Farao akamwambia Yusufu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yusufu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la vita kama msaidizi wake; watu wakamtangulia wakipaza sauti na kusema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alimweka Yusufu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri. Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” Farao akamwita Yusufu jina Safenath-Panea; pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yusufu akaitembelea nchi yote ya Misri.