Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:28-45

Mwanzo 41:28-45 Biblia Habari Njema (BHN)

Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri. Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii. Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni. “Kwa hiyo yafaa sasa, ee Farao, umteue mtu mwenye ujuzi na hekima, umpe jukumu la kuiangalia nchi yote ya Misri. Tena, ee Farao, uwateue wasimamizi kadhaa hapa nchini, uwaagize wakusanye sehemu ya tano ya mavuno yote ya Misri katika kipindi hiki cha miaka saba ya shibe. Uwaagize wasimamizi hao wakusanye chakula chote katika miaka saba ijayo ya mavuno kwa wingi. Nafaka hiyo na iwekwe chini ya mamlaka yako, ee Farao, iwe akiba ya chakula kwa miji yote, nao waitunze nafaka hiyo. Chakula hicho kitakuwa akiba ya kinga kwa nchi ya Misri isije ikaangamia kutokana na njaa ya miaka saba itakayofuata.” Shauri alilotoa Yosefu lilionekana kuwa jema mbele ya Farao na watumishi wake wote. Kwa hiyo Farao akawauliza watumishi wake, “Huyu mtu ana roho ya Mungu! Je, tunaweza kumpata mtu mwingine kama huyu?” Kisha akamwambia Yosefu, “Kwa kuwa Mungu amekufunulia haya yote, hakuna mtu mwingine mwenye busara na hekima kama wewe. Wewe ndiwe utakayeisimamia nchi yangu, na watu wangu wote watakuwa chini ya amri yako. Mimi tu ndiye mkuu kuliko wewe kwa kuwa nakalia kiti cha kifalme. Basi, sasa nakuteua rasmi kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri!” Ndipo, Farao akaivua pete yake ya mhuri kidoleni mwake na kumvisha Yosefu, akamvalisha na mavazi ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni. Farao akampandisha katika gari lake la pili la farasi na walinzi wakatangulia mbele ya Yosefu wakipaza sauti na kusema, “Pigeni magoti!” Ndivyo Farao alivyompa Yosefu madaraka makubwa juu ya nchi yote ya Misri. Zaidi ya hayo, Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ndimi Farao! Nasema: Mtu yeyote katika nchi nzima ya Misri asiinue mkono wala mguu wake bila kibali chako.” Farao akampa Yosefu jina la Kimisri: Safenath-panea. Akamwoza Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Basi, Yosefu akaanza kuitembelea nchi nzima ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 41

Mwanzo 41:28-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa kali sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumishi wake wote. Farao akawaambia watumishi wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye Roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa msimamizi wa nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya mhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe. Na Yusufu akaenda huku na huko katika nchi yote ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 41

Mwanzo 41:28-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 41

Mwanzo 41:28-45 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

“Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri, lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi. “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni. “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe. Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.” Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. Hivyo Farao akawauliza, “Je, tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, aliye na Roho wa Mungu ndani yake?” Ndipo Farao akamwambia Yusufu, “Maadamu Mungu amekufunulia haya yote, hakuna yeyote mwenye akili na hekima kama wewe. Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.” Kwa hiyo Farao akamwambia Yusufu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yusufu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la vita kama msaidizi wake; watu wakamtangulia wakipaza sauti na kusema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alimweka Yusufu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri. Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” Farao akamwita Yusufu jina Safenath-Panea; pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yusufu akaitembelea nchi yote ya Misri.

Shirikisha
Soma Mwanzo 41