Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 31:31-42

Mwanzo 31:31-42 NENO

Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyang’anya binti zako kwa nguvu. Lakini ukimkuta yeyote na miungu yako, huyo mtu hataishi. Mbele ya jamaa zetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho; kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiiba hiyo miungu. Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo, na ndani ya hema la Lea, na ndani ya hema la wajakazi wale wawili, lakini hakuipata hiyo miungu. Baadaye alipotoka hema la Lea, akaingia hema la Raheli. Basi Raheli ndiye alikuwa ameichukua ile miungu ya nyumbani mwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia, na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote. Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike bwana wangu, kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani mwake. Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda? Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote, umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu. “Hadi sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako. Sijakuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, bali nimegharimia hasara mwenyewe. Tena umenidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku. Hali yangu imekuwa hivi: Nimechomwa kwa joto la mchana, na kupigwa na baridi usiku, pia usingizi ulinipotea. Imekuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi. Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”