Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 30:25-43

Mwanzo 30:25-43 NENO

Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu. Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua kazi niliyokufanyia.” Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa uaguzi kwamba Mwenyezi Mungu amenibariki kwa sababu yako.” Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.” Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi nimekutumikia na jinsi wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu. Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Mwenyezi Mungu amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?” Labani akamuuliza, “Nikupe nini?” Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote, lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako. Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabaka mabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi, na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabaka mabaka. Hawa watakuwa ujira wangu. Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabaka mabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.” Labani akasema, “Ninakubali; na iwe kama ulivyosema.” Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa, na mbuzi jike wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao), na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe. Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu, naye Yakobo akaendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki. Lakini Yakobo akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. Kisha akaweka fito hizo katika mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu, wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabaka mabaka. Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani. Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito, lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo. Hivyo Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, mjakazi na watumishi, na ngamia na punda.