Mwanzo 29:13-30
Mwanzo 29:13-30 NEN
Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani kwake, kisha Yakobo akamwambia mambo yote. Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni nyama yangu na damu yangu mwenyewe.” Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima, Labani akamwambia, “Kwa vile wewe ni jamaa yangu, ndiyo sababu unifanyie kazi bila ujira? Niambie ujira wako utakuwa nini.” Labani alikuwa na binti wawili, binti mkubwa aliitwa Lea na binti mdogo aliitwa Raheli. Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura. Yakobo akampenda Raheli, akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.” Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote. Kaa pamoja na mimi hapa.” Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli. Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka nikutane naye kimwili.” Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu. Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili. Naye Labani akamtoa Zilpa, mtumishi wake wa kike, kuwa mtumishi wa Lea, binti yake. Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?” Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa. Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.” Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake. Labani akamtoa Bilha mtumishi wake wa kike kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake. Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.