Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 26:12-35

Mwanzo 26:12-35 NEN

Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu BWANA alimbariki. Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” Basi Isaki akatoka huko akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. Ndipo Isaki akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya kufa Abrahamu, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa. Watumishi wa Isaki wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaki wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna. Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.” Kutoka pale akaenda Beer-Sheba. Usiku ule BWANA akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Abrahamu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe, nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.” Isaki akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima. Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake. Isaki akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu na ninyi mlinichukia na kunifukuza?” Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa BWANA alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu, kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe kwamba hutatudhuru, kama jinsi nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote na kuwaondoa kwetu kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na BWANA.’ ” Basi Isaki akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa. Kesho yake asubuhi na mapema, wakaapizana wao kwa wao. Kisha Isaki akawaruhusu waende zao, wakamwacha Isaki kwa amani. Siku hiyo watumishi wa Isaki wakaja wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!” Naye akakiita Shiba, mpaka leo mji huo unaitwa Beer-Sheba. Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti. Hawa walikuwa chanzo cha huzuni ya Isaki na Rebeka.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 26:12-35