Mwanzo 2:7-17
Mwanzo 2:7-17 NENO
Bwana Mwenyezi Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai. Basi Bwana Mwenyezi Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni; huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. Bwana Mwenyezi Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Mti wa uzima ulikuwa katikati ya bustani, na pia mti wa kujua mema na mabaya. Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni; kuanzia hapo ukagawanyika kuwa mito minne. Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri; bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati. Bwana Mwenyezi Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. Bwana Mwenyezi Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani; lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”