Mwanzo 19:1-11
Mwanzo 19:1-11 NEN
Malaika wale wawili wakafika Sodoma wakati wa jioni, naye Loti alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Wakati alipowaona, aliondoka kwenda kuwalaki na kuwasujudia hadi chini. Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.” Wakamjibu, “La hasha, tutalala hapa nje uwanjani.” Lakini akasisitiza kwa nguvu kwamba waingie pamoja naye nyumbani kwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala. Kabla hawajaenda kulala, watu wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba. Wakamwita Loti wakisema, “Wako wapi wale watu ambao walikuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuweze kuwalawiti.” Loti akatoka nje kuonana nao, akaufunga mlango nyuma yake, akasema, “La hasha, rafiki zangu. Msifanye jambo hili ovu. Tazama, ninao binti wawili ambao kamwe hawajakutana kimwili na mwanaume. Acha niwatoe nje kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote watu hawa, kwa sababu wako kwenye ulinzi chini ya dari langu.” Wakamjibu, “Tuondokee mbali.” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Loti na kusonga mbele ili kuvunja mlango. Lakini watu wale waliokuwa ndani wakanyoosha mkono wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kufunga mlango. Kisha wakawapiga kwa upofu wale watu waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.