Mwanzo 17:1-14
Mwanzo 17:1-14 NENO
Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi Mungu akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; nenda mbele zangu na uishi kwa unyofu. Nitafanya agano kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana.” Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, “Kwangu mimi, hili ndilo agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. Hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Ibrahimu, kwa maana nimekufanya baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana; kwako yatatoka mataifa, na wafalme watatoka kwako. Nitalithibitisha agano langu kama agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo, nami nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazao wako. Nchi yote ya Kanaani, unayoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na ya uzao wako; nami nitakuwa Mungu wao.” Ndipo Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwako wewe, lazima ushike agano langu, wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo. Hili ni agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa, na hii itakuwa ni alama ya agano kati yangu na ninyi. Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio wa uzao wako. Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima atahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni agano la milele. Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.”