Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 17:1-14

Mwanzo 17:1-14 NEN

Abramu alipokuwa na miaka tisini na tisa, BWANA akamtokea akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; enenda mbele zangu na uishi kwa unyofu. Nami nitafanya Agano langu kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.” Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, “Kwa upande wangu, hili ndilo Agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako. Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako. Nchi yote ya Kanaani, unakoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na uzao wako, nami nitakuwa Mungu wao.” Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi. Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio watoto wako. Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima watahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni Agano la milele. Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake, amelivunja Agano langu.”