Mwanzo 12:10-20
Mwanzo 12:10-20 NENO
Basi kulikuwa na njaa katika nchi hiyo, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali. Alipokaribia kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura. Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Kisha wataniua, lakini wewe watakuacha hai. Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yahifadhiwe kwa sababu yako.” Abramu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana wa sura. Maafisa wa Farao walipomwona, wakamsifia kwa Farao; ndipo Sarai akapelekwa kwa nyumba ya mfalme. Kwa ajili ya Sarai, Farao akamtendea Abramu mema, naye Abramu akapata kondoo, ng’ombe, punda, ngamia, na watumishi wa kiume na wa kike. Lakini Mwenyezi Mungu akamwadhibu Farao na nyumba yake kwa maradhi ya kufisha kwa sababu ya kumchukua Sarai, mke wa Abramu. Ndipo Farao akamwita Abramu, akamuuliza, “Umenifanyia nini? Kwa nini hukuniambia yeye ni mke wako? Kwa nini ulisema, ‘Yeye ni dada yangu,’ hata nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa basi, mke wako huyu hapa. Mchukue uende zako!” Kisha Farao akawapa watu wake amri kuhusu Abramu, wakamsindikiza pamoja na mke wake na kila alichokuwa nacho.