Wagalatia 3:6-14
Wagalatia 3:6-14 NENO
Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. Andiko liliona tangu awali kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, hivyo likatangulia kumtangazia Abrahamu Injili, likisema kwamba, “Kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani. Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” Alitukomboa ili baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kupitia kwa Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.