Wagalatia 2
2
Paulo akubaliwa na mitume
1Kisha, baada ya miaka kumi na nne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu, wakati huu pamoja na Barnaba, na nikamchukua Tito pia. 2Nilienda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. 3Lakini hata Tito aliyekuwa nami, na alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. 4Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru tulio nao katika Al-Masihi Isa, wapate kututia utumwani, 5hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili ukweli wa Injili ubaki nanyi.
6Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote. 7Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. 8Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. 9Basi Yakobo, Kefa#2:9 yaani Petro na Yohana, walioonekana kama nguzo za jumuiya ya waumini, walitupatia mkono wa shirika, mimi na Barnaba, walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa, na wao waende kwa Wayahudi. 10Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
Paulo ampinga Petro huko Antiokia
11Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. 12Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. 13Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.
14Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?
Wayahudi na watu wa Mataifa wanaokolewa kwa imani
15“Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16bado tunajua kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kupitia kwa imani katika Isa Al-Masihi. Hivyo sisi pia, tumemwamini Al-Masihi Isa ili tupate kuhesabiwa haki kupitia kwa imani katika Al-Masihi, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
17“Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Al-Masihi, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Al-Masihi amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! 18Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonesha kwamba mimi ni mkosaji. 19Kwa maana mimi kupitia kwa sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20Nimesulubiwa pamoja na Al-Masihi, wala si mimi tena ninayeishi, bali Al-Masihi ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani katika Mwana wa Mungu#2:20 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kupitia kwa Torati, basi Al-Masihi alikufa bure!”
Iliyochaguliwa sasa
Wagalatia 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.