Ezekieli 7:1-13
Ezekieli 7:1-13 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa nchi ya Israeli: “ ‘Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi! Sasa mwisho umekuja juu yenu, nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza. Sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Hakika nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa! Tazama, yanakuja! Mwisho umewadia! Mwisho umewadia! Umejiinua wenyewe dhidi yenu. Tazama, umewadia! Maangamizi yamekuja juu yenu, ninyi mnaoishi katika nchi. Wakati umewadia! Siku imekaribia! Kuna hofu kuu ya ghafula juu ya milima, wala si furaha. Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu na kumaliza hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo. Sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi za machukizo miongoni mwenu. “ ‘Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ambaye huwapiga. “ ‘Tazama, siku imefika! Tazama, imewadia! Maangamizi yamezuka ghafula, fimbo imechanua, nayo majivuno yamechipua! Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu waovu. Hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi hilo: hakuna utajiri wao utabaki, wala chochote cha thamani. Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote. Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai. Kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake.