Ezekieli 6:1-14
Ezekieli 6:1-14 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema, “Mwanadamu, elekeza uso wako kukabili milima ya Israeli, utabiri dhidi yake, useme, ‘Ee milima ya Israeli, sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi. Hili ndilo neno asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa milima na vilima, magenge na mabonde: Nakaribia kuleta upanga dhidi yenu, na nitapaharibu mahali penu pa juu pa kuabudia. Madhabahu yenu yatabomolewa na madhabahu yenu ya kufukizia uvumba yatavunjavunjwa, nami nitawachinja watu wenu mbele ya sanamu zenu. Nitazilaza maiti za Waisraeli mbele ya sanamu zao, nami nitatawanya mifupa yenu kuzunguka madhabahu yenu. Popote mnapoishi, miji itaangamizwa na mahali pa juu patabomolewa, ili madhabahu zenu ziharibiwe na kuteketezwa; sanamu zenu zitavunjwavunjwa na kuharibiwa, madhabahu zenu za kufukizia uvumba zitabomolewa, na kila mlichokifanya kitakatiliwa mbali. Watu wenu watachinjwa kati yenu, nanyi mtatambua Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. “ ‘Lakini nitawabakiza hai baadhi yenu, kwa kuwa baadhi yenu watanusurika kuuawa kwa upanga watakapokuwa wametawanyika katika nchi na katika mataifa. Ndipo katika mataifa walikochukuliwa mateka, watakaonusurika watanikumbuka. Watakumbuka jinsi nilivyohuzunishwa na mioyo yao ya uzinzi ambayo imegeuka kuwa mbali nami, na kwa macho yao ambayo yametamani sanamu zao. Watajichukia wenyewe kwa sababu ya uovu walioutenda na desturi zao za kuchukiza. Nao watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, sikuwaonya bure kuwa nitaleta maafa hayo yote juu yao. “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Piga makofi, pigisha mguu wako chini, na upige kelele useme, “Ole!” kwa sababu ya maovu yote na desturi za kuchukiza za nyumba ya Israeli, wataangamia kwa upanga, njaa na tauni. Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni, naye aliye karibu atauawa kwa upanga, naye yule atakayenusurika na kubaki atakufa kwa njaa. Hivyo ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao. Nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wakati maiti za watu wao zitakapokuwa zimelala kati ya sanamu zao kuzunguka madhabahu yao, juu ya kila kilima kilichoinuka na juu ya vilele vyote vya milima, chini ya kila mti uliotanda na kila mwaloni wenye majani, yaani sehemu walizofukizia uvumba kwa sanamu zao zote. Nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yao na kuifanya nchi yao ukiwa, kuanzia jangwani hadi Dibla, kila mahali wanapoishi. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”