Ezekieli 41
41
1Kisha yule mtu akanileta katika ukumbi mkuu, naye akaipima miimo; upana wake ulikuwa dhiraa sita#41:1 Dhiraa 6 ni sawa na mita 2.7. kila upande. 2Ingilio lilikuwa la upana wa dhiraa kumi, na kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa tano. Pia akapima ukumbi mkuu; ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini#41:2 Dhiraa 40 ni sawa na mita 18., na upana wa dhiraa ishirini.
3Kisha akaingia mahali patakatifu na kupima miimo ya ingilio, kila mmoja ulikuwa na upana wa dhiraa mbili. Ingilio lilikuwa na upana wa dhiraa sita, na kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa saba#41:3 Dhiraa 7 ni sawa na mita 3.15.. 4Naye akapima urefu wa mahali patakatifu; ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini hadi mwisho wa sehemu ya nje ya ukumbi mkuu. Akaniambia, “Hapa ndipo Patakatifu pa Patakatifu.”
5Kisha akapima ukuta wa Hekalu, nao ulikuwa na unene wa dhiraa sita, na kila chumba cha pembeni kuzunguka Hekalu kilikuwa na upana wa dhiraa nne. 6Vyumba vya pembeni vilikuwa na ghorofa tatu, kimoja juu ya kingine, kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Kulikuwa na boriti katika ukuta wote wa Hekalu ili kuimarisha vyumba vya pembeni; kwa hiyo boriti hizo hazikushikamanishwa kwenye ukuta wa Hekalu. 7Vyumba vya pembeni vilivyozunguka Hekalu vilizidi kupanuka kulingana na sakafu zilivyoenda juu. Ujenzi uliozunguka Hekalu ulijengwa kukwea juu, kwa hiyo vyumba vilipanuka kwa kadiri ya kila kimoja kilivyoenda juu. Ngazi za kupandia zilianzia sakafu ya chini hadi sakafu ya juu kabisa kupitia kwa sakafu ya kati.
8Nikaona kwamba Hekalu lilikuwa na kitako kilichoinuliwa pande zote; huu ukawa msingi wa vile vyumba vya pembeni. Ulikuwa na urefu wa ule ufito mmoja wa kupimia, yaani dhiraa ndefu sita. 9Ukuta wa nje wa vyumba vya pembeni ulikuwa na unene wa dhiraa tano. Eneo la wazi katikati ya vyumba vya pembeni vya Hekalu 10na vyumba vya makuhani lilikuwa na upana wa dhiraa ishirini kuzunguka Hekalu pande zote. 11Kulikuwa na maingilio kwenye vyumba vya pembeni kutokea eneo lililo wazi, moja upande wa kaskazini na lingine upande wa kusini, nao msingi uliounganisha lile eneo la wazi ulikuwa na upana wa dhiraa tano ukilizunguka lote.
12Jengo lililoelekeana na ua wa Hekalu upande wa magharibi lilikuwa na upana wa dhiraa sabini. Ukuta wa jengo hilo ulikuwa na unene wa dhiraa tano, kulizunguka lote, urefu ulikuwa wa dhiraa tisini#41:12 Dhiraa 90 ni sawa na mita 40.5..
13Kisha akapima Hekalu; lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na ua wa Hekalu na jengo pamoja na kuta zake vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja pia. 14Upana wa ua wa Hekalu upande wa mashariki, pamoja na upande wa mbele wa Hekalu ulikuwa dhiraa mia moja.
15Kisha akapima urefu wa jengo lililoelekeana na ua upande wa nyuma wa Hekalu, pamoja na baraza zake kila upande, kwa kipimo cha dhiraa mia moja.
Ukumbi mkuu, na mahali patakatifu, pamoja na baraza inayoelekeana na ukumbi, 16pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta hadi kwenye madirisha, na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao. 17Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la mahali patakatifu, na katika kuta zilizozunguka mahali patakatifu na sehemu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa, 18kulinakshiwa makerubi na mitende; mtende ulikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili: 19upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote. 20Kuanzia sakafu hadi eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na mitende, pamoja na kwenye ukuta wa nje wa Patakatifu.
21Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba; na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulifanana na huo. 22Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza iliyo mbele za Mwenyezi Mungu.” 23Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili. 24Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango. 25Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na mitende kama nakshi zilizokuwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioning’inia mbele ya baraza kwa nje. 26Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 41: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.