Ezekieli 39
39
Majeshi ya Gogu yataangamizwa
1“Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali. 2Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli. 3Kisha nitaupiga upinde wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume. 4Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama pori. 5Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 6Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
7“ ‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndimi Aliye Mtakatifu wa Israeli. 8Hili jambo linakuja! Hakika litatendeka, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.
9“ ‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni. 10Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali ya wale waliochukua mali yao nyara, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
11“ ‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki mwa Bahari. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu#39:11 maana yake Makundi ya Gogu.
12“ ‘Kwa miezi saba nyumba ya Israeli itakuwa ikiwazika ili kuisafisha nchi. 13Watu wote wa nchi watawazika, nayo siku nitakayotukuzwa itakuwa siku ya kumbukumbu kwa ajili yao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
14“ ‘Watu wataajiriwa mara kwa mara kuisafisha nchi. Baadhi yao watapita nchini kote, na, wakiwa na wengine, watawazika wale waliosalia juu ya ardhi. Mwisho wa hiyo miezi saba wataanza upekuzi wao. 15Wanapopita nchini kote, na mmoja wao akaona mfupa wa mwanadamu, ataweka alama kando yake hadi wachimba kaburi wauzike katika Bonde la Hamon-Gogu. 16(Pia mji uitwao Hamona#39:16 maana yake Kundi utakuwa humo.) Hivyo ndivyo watakavyoisafisha nchi.’
17“Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ita kila aina ya ndege na wanyama pori wote, waambie: ‘Kusanyikeni mje pamoja kutoka pande zote kwa ajili ya dhabihu ninayowaandalia, dhabihu kuu katika milima ya Israeli. Huko mtakula nyama na kunywa damu. 18Mtakula nyama za watu mashujaa na kunywa damu za wakuu wa dunia kana kwamba ni za kondoo dume na kondoo wake, mbuzi na mafahali, wote walionona kutoka Bashani. 19Katika dhabihu ninayoandaa kwa ajili yenu, mtakula mafuta hadi mshibe, na kunywa damu hadi mlewe. 20Kwenye meza yangu watajishibisha kwa farasi na wapanda farasi, watu mashujaa na askari wa kila aina,’ asema Bwana Mungu Mwenyezi.
21“Nitauonesha utukufu wangu miongoni mwa mataifa, nayo mataifa yote wataiona adhabu nitakayotoa na mkono wangu nitakaouweka juu yao. 22Kuanzia siku ile na kuendelea nyumba ya Israeli itajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao. 23Na mataifa watajua kuwa nyumba ya Israeli walienda utumwani kwa ajili ya dhambi yao, kwa sababu hawakuwa waaminifu kwangu. Hivyo niliwaficha uso wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga. 24Niliwatendea sawasawa na uchafu wao na makosa yao, nami nikawaficha uso wangu.
25“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Sasa nitamrudisha Yakobo kutoka utumwani, nami nitawahurumia watu wote wa Israeli, nami nitakuwa na wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu. 26Wataisahau aibu yao na jinsi walivyoonesha kutokuwa waaminifu kwangu mimi wakati waliishi salama katika nchi yao, bila kuwa na mtu yeyote wa kuwatia hofu. 27Nitakapokuwa nimewarudisha kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za adui zao, mimi nitajionesha kuwa mtakatifu kupitia kwao machoni mwa mataifa mengi. 28Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao, ingawa niliwapeleka uhamishoni miongoni mwa mataifa, nitawakusanya tena katika nchi yao wenyewe, bila kumwacha yeyote nyuma. 29Sitawaficha tena uso wangu, kwa maana nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 39: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.