Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 14:12-23

Ezekieli 14:12-23 NEN

Neno la BWANA likanijia kusema, “Mwanadamu, kama nchi itanitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikinyoosha mkono wangu dhidi yake kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, hata kama watu hawa watatu: Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, ndio hao tu wangeweza kujiokoa wenyewe kwa uadilifu wao, asema BWANA Mwenyezi. “Au kama nikipeleka wanyama pori katika nchi hiyo yote na kuifanya isiwe na watoto, nayo ikawa ukiwa kwamba hakuna mtu apitaye katika nchi hiyo kwa sababu ya wanyama pori, hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa. “Au kama nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikiua watu wake na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa. “Au kama nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kwa njia ya kumwaga damu, kuua watu wake na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, hata kama Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao. “Kwa maana hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani, upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! Lakini watakuwepo wenye kuokoka, wana na binti wataletwa kutoka nje ya nchi hiyo. Watawajia ninyi, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya yale yote niliyoleta juu yake. Mtafarijika wakati mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwa kuwa mtajua kwamba sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema BWANA Mwenyezi.”