Ezekieli 11:14-25
Ezekieli 11:14-25 NEN
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema, ‘Wako mbali na BWANA; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’ “Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, lakini kwa kitambo kidogo mimi nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizokwenda.’ “Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawakusanyeni kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’ “Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za machukizo. Nitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema BWANA Mwenyezi.” Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Basi utukufu wa BWANA ukapaa juu kutoka mji, ukatua juu ya mlima ulio upande wa mashariki ya mji. Roho akaniinua na kunileta mpaka kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu. Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka, nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu BWANA alichokuwa amenionyesha.