Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 11:1-25

Ezekieli 11:1-25 NENO

Ndipo Roho akaniinua na kunileta hadi kwenye lango la nyumba ya BWANA linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango palikuwa na wanaume ishirini na watano. Nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu. BWANA akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu. Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’ Kwa hiyo tabiri dhidi yao; tabiri, ewe mwanadamu.” Kisha Roho wa BWANA akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo asemalo BWANA: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu. Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti. “Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Maiti mlizozitupa huko ndizo nyama, na mji huu ndio chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko. Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta dhidi yenu, asema BWANA Mwenyezi. Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu. Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA. Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.” Basi nilipokuwa nikitoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, “Ee BWANA Mwenyezi! Je, utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?” Neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu nawe pamoja na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema kuwahusu, ‘Wako mbali na BWANA; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’ “Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, hata hivyo, kwa kitambo kidogo, nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizoenda.’ “Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Nitawakusanya kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’ “Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za kuchukiza. Nitawapa moyo usiogawanyika na kuweka roho mpya ndani yao; nitaondoa ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za kuchukiza, nitawalipa kikamilifu kulingana na matendo yao,” asema BWANA Mwenyezi. Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Basi utukufu wa BWANA ukapaa juu kwanzia katika mji na kutua juu ya mlima ulio mashariki mwa mji. Roho akaniinua na kunileta kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu. Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka, nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu BWANA alichokuwa amenionesha.