Ezekieli 10
10
Utukufu unaondoka Hekaluni
1Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. 2Mwenyezi Mungu akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia kati ya yale magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka kati ya makerubi na ukayatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani.
3Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani. 4Kisha utukufu wa Mwenyezi Mungu ukainuka kutoka juu ya wale makerubi, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mng’ao wa utukufu wa Mwenyezi Mungu. 5Sauti ya mabawa ya wale makerubi ilisikika hadi ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi#10:5 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote). anapoongea.
6Mwenyezi Mungu alimwamuru yule mtu aliyevaa nguo ya kitani, akisema, “Chukua moto toka kati ya magurudumu, miongoni mwa makerubi.” Basi yule mtu aliingia ndani, akasimama pembeni mwa gurudumu. 7Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao, akauchukua moto. Akautia mikononi mwa yule mtu aliyevaa nguo ya kitani, naye alipoupokea, akatoka nje. 8(Chini ya mabawa ya makerubi palionekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.)
9Nikatazama, nikaona magurudumu manne kando ya makerubi, moja kando ya kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama zabarajadi. 10Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana; kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine. 11Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale makerubi. Makerubi walipoenda, magurudumu hayakuzunguka. Makerubi walienda upande wowote ule kichwa kilielekea, pasipo kugeuka. 12Miili yao: migongo yao, mikono na mabawa yao, ilikuwa imejaa macho kote, pamoja na yale magurudumu manne. 13Nikasikia magurudumu yakiitwa “magurudumu ya kisulisuli”. 14Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba, na uso wa nne ulikuwa wa tai.
15Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari. 16Makerubi walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalienda; na makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka ardhini, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwa makerubi. 17Makerubi waliposimama, nayo pia yalitulia; nao makerubi walipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu hayo.
18Kisha utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi. 19Nilipokuwa nikitazama, makerubi wakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda, yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi Mungu; nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao.
20Hawa walikuwa viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua kuwa hao walikuwa makerubi. 21Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne, na chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu. 22Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alienda mbele moja kwa moja.
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.